Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Kashif Virk, mtaalamu wa masuala ya dini na Mwislamu wa Sweden, pamoja na kundi la Waislamu, waliamua kuanzisha kampeni yenye kaulimbiu “Muulize Mwislamu!”, kwa lengo la kukabiliana na propaganda dhidi ya Uislamu zinazoendeshwa na wanasiasa wenye misimamo mikali nchini Sweden na kuzuia kuenea chuki dhidi ya Uislamu.
Bi. Munira Niazi, ambaye ni miongoni mwa washiriki wa kampeni hiyo, alisema: “Hili ni sanduku la Pandora ambalo serikali imeliweka kwa sera zake za misimamo mikali. Katika serikali iliyopita, waziri mkuu mwenye fikra za mrengo mkali wa kulia alijaribu kutekeleza sera zinazopinga Uislamu na uhamiaji.”
Aliongeza kuwa; hali hiyo ilifikia hatua ambapo matatizo yote ya jamii, yakiwemo umaskini, kupanda kwa gharama za maisha na ukosefu wa uwiano katika baadhi ya maeneo, vilihusishwa na Waislamu, watu wa makundi madogo na wahamiaji, badala ya kuchukua hatua za kuyatatua.
Bw. Virk pia alisema: “Kwa masikitiko, tunaona kwamba kila wakati wanapohitaji kutumia kadi ya chuki dhidi ya Uislamu, huitumia ili kufikia malengo yao.”
Madhara ya hali hiyo yameonekana kwa kiwango kikubwa, mwaka uliopita, mtu mwenye silaha aliwaua watu 10 katika mji wa Örebro nchini Sweden, wengi wao wakiwa na historia ya uhamiaji. Kote nchini Sweden, misikiti imekuwa ikiharibiwa mara kwa mara, na mwaka 2023 nchi hiyo ilikabiliwa na wimbi la maandamano ambapo nakala za Qur’ani zilichomwa moto au kufanyiwa vitendo vya kidhalili kwa namna mbalimbali, jambo hili lilikuwa la kusikitisha na la kutia wasiwasi sana.
Chanzo: Imenukuliwa kutoka ripoti ya The Guardian.
Maoni yako